Siri ya kuwa na mwaka 2019 bora zaidi!

Hatua 4 zitakazokusaidia kutimiza malengo yako

Siri ya kuwa na mwaka 2019 bora zaidi!

Ninapenda mwanzo wa mwaka mpya! Kila Januari, mimi hupata hisia hii ya “jambo lolote linawezekana” na ninajawa na hamu na nguvu ya kufanya mambo mapya ya kusisimua! Lakini kwa kweli, nilianza kuhisi hivi mwaka uliopita wakati mwalimu wetu wa sayansi, Bw. Majambo, alipotufunza mbinu ya kuwa na mwaka mpya bora zaidi.

Katika darasa letu la kwanza la muhula mpya, Bw. Majambo alituambia tuandike ndoto zetu kubwa tulizotaka kutimiza mwaka huo. Nikafikiria, “Ninataka kumjengea mama yangu nyumba, ninataka kuwa na gari na niliendeshe mwenyewe na ninataka kusafiri hadi nchi nyingine kwa ajili ya kujifurahisha lakini siwezi kutimiza haya yote kwa mwaka mmoja!”

Kwa hiyo nikamuomba Bw. Majambo usaidizi. Aliniambia nifikirie kuhusu jambo litakalonisaidia kutimiza ndoto hizi zingine kubwa lakini lilikuwa linawezekana kuanza leo. Kwa hiyo nikafikiria, “Sayansi ni somo ninalolipenda, labda siku moja nitakuwa mwanasayansi na nipate pesa ninazohitaji kununua nyumba, gari na kusafiri.” Ninaloweza kufanya sasa ni kujiunga na kundi la sayansi na pengine nijaribu kushinda shindano la sayansi la kanda.

Rafiki yangu Aminatou alijiunga na kundi hilo pamoja nami. Tulisuluhisha matatizo pamoja baada ya shule na tukakutana wikendi kujipima. Sisi ndio tulikuwa wasichana pekee kwenye kikundi na wavulana walituangalia kana kwamba sisi sio werevu kama wao. Hatimaye, tulianza kujibu maswali haraka kuliko wao na wakaanza kutuheshimu.

Kundi letu lilihitimu kwenda kwenye shindano la sayansi la kanda na likawa la tatu kati ya timu 10. Hili lilinionyesha kwamba ninaweza kufanya lolote nikijitahidi na kujiamini. Hakuna lengo ambalo ni kubwa sana kwangu sasa – mwaka huu, nina uhakika kwamba tutaweza kufika hadi mashindano ya kitaifa.