Tambua na Ukomeshe: Habari za Kweli dhidi ya Habari Bandia!

Tunaweza kupitia hii, makala moja baada ya nyingine!

Tambua na Ukomeshe: Habari za Kweli dhidi ya Habari Bandia!

Tangu niliposikia mara ya kwanza kuhusu janga kuu la hivi sasa, nilihisi kama siwezi kuepuka ripoti za taarifa, uvumi, na ushauri wa kiafya kuhusu virusi hivi.

Ziko kwenye Runinga! Ziko kwenye mitandao ya kijamii! Ziko hata kwenye kikundi changu cha gumzo cha darasa langu! Sina uhakika kuhusu ninachopaswa kuamini kwa kuwa kuna habari nyingi sana na nyingi zinasikika kama zinawezakuwa za ukweli.

Wakati ambapo sijui ninachopaswa kufanya, kuna mtu mmoja ambaye ninajua ninaweza kumgeukia: dada yangu mdogo. Nilimuuliza kuhusu jinsi ambavyo ninaweza kutambua kilicho cha kweli na kile ambacho ni cha mzaha na akanipa ushauri mwema. Haya ndiyo aliyoniambia:

Tafuta kwa bidii!

Jambo la kwanza ni kuchunguza chanzo cha habari hizi. Je, zinatoka kwa serikali au kwa shirika kama vile Shirika la Afya Duniani (WHO)? Ikiwa zimetoka kwa tovuti ya habari, ni ambayo umewahi kuisikia? Iwapo hujui chanzo cha habari hii, basi ni wazo nzuri kuwa na shaka.

Psst: Je, unafahamu WHO ni nini? WHO ni shirika la afya ya umma la kimataifa na sehemu ya Umoja wa Mataifa. Tunaweza kuamini habari inayotoka kwa WHO kwa sababu huwa na viwango madhubuti na machapisho yao huzingatia misingi ya kauli zinazotokana na utafiti mpana.

Mwandishi ni nani?

Kila unaposoma makala, unaweza kutazama kitengo cha ‘kuhusu mwandishi’ ili usome habari kumhusu, au unaweza kutafuta jina lake kutoka kwa Google ili kujua yeye ni nani na hati zake za utambulisho. Kuwa mwangalifu! Kwa kuwa tu mwandishi anasema kuwa yeye ni Daktari haimaanishi kuwa hakika yeye ni daktari, huenda akawa sio mtaalamu kuhusu eneo analoandika.

Sio mzaha

Kunazo tovuti nyingi na wasifu za mitandao ya kijamii ambazo huandaa 'habari bandia' kama mzaha au kwa ajili ya kujiburudisha. Unaposoma makala (hasa ile inayoonekana kuwa mbaya!), chunguza uone iwapo makala hiyo ilitoka kwa tovuti au blogi ya tashtiti au vichekesho. KIDOKEZO-KUTOKA KWA MTAALAMU Unapokuwa kwenye Facebook, huenda ukaona arifa kando ya viungo vilivyoshirikiwa inayokwambia iwapo makala ni ya utani au mzaha. Arifa hizo ni za kuaminika na ni kipengele kizuri cha kukusaidia kutambua kati ya ukweli na uongo.

Yaangalie!

Maelezo madogo ni ya muhimu. Iwapo mtu atakutumia picha iliyopigwa kutoka kwa skrini au ujumbe uliosambazwa, muombe kiungo cha chanzo asili. Iwapo huwezi kupata kiungo asili, bado unaweza kuitafuta kwenye mtandao ili uone iwapo unaweza kupata habari sawa au taarifa kutoka kwa vyanzo vya kuheshimika. Iwapo huwezi, kuna uwezekano mzuri kuwa huenda ikawa ni mzaha.

Kwa kuwa sasa una vidokezi hivi, unaweza kuanza kutambua taarifa bandia na kusaidia kukomesha ueneaji wa habari potofu. Iwapo utaona makala au kupata ujumbe ambao unaonekana kuwa mzaha, usiushiriki na usiwe muoga sana wa kuwajulisha marafiki na jamaa zako kuwa wanapaswa kuacha kuushiriki pia.