Kuwa rafiki wa dhati na mama yangu

Haikuwa rahisi lakini sasa ni jambo la busara.

Kuwa rafiki wa dhati na mama yangu

Mimi na mama yangu ni watu tofauti kabisa; anapenda msimu wa baridi, napenda msimu wa joto, anapendelea chai bila maziwa, napendelea kuongeza maziwa na sukari. Kwa ujumla, huwa hatukubaliani kwa chochote kile.

Hii ilikuwa ikinikatisha tamaa sana. Nilianza kuamini kwamba singeweza kuongea na yeye kuhusu kitu chochote.

Marafiki wangu wangeniambia kuhusu wanavyoongea na mama zao kuhusu mambo ambayo singeweza kumwelezea mama yangu - kama vile mahusiano na shule, nilikuwa nikihisi ni kama hawezi kuelewa.

Hata hivyo nilielewana vizuri na shangazi yangu. Kwa hivyo siku moja nikaongea na yeye kuhusu uhusiano wangu na mama yangu wenye changamoto. Kwa mshangao wangu, alinielezea kwamba mama yangu alikuwa akihisi hivyo pia; alitaka kuwa karibu na mimi lakini hakuwa na uhakika kuhusu jinsi ya kuwasiliana na mimi na kuzungumza na mimi kuhusu mambo kama vile wavulana na kazi ya shule.

Shangazi yangu alinishauri nipange siku maalum kwangu na mama yangu ambayo tunaweza kufahamiana. Alinifafanulia kwamba kama ninataka kuwa karibu na mama yangu ninapaswa:

  • kuongea na yeye kwa njia ya kirafiki na ya heshima. Nifikirie ninachotaka kupata kutoka kwa mazungumzo na ni hakikishe nimesikiliza maoni yake anapoongea pia.
  • kupanga kuzungumza na yeye wakati itakuwa ni sisi nyumbani peke yetu. Kwa njia hiyo ataweza kunipa muda wake bila kutatizwa na wengine.
  • kufanya kitu ambacho wote tunafurahia, kama vile kutazama maonyesho tuyapendayo ya TV au kushughulikia bustani. Hii itasaidia kuondoa vizuizi vyovyote na kufanya mazungumzo kuwa rahisi.

Nikiwa nimeridhika, nilirudi nyumbani na kuanza kutumia ushauri wa shangazi wangu. Nikapanga tarehe nyumbani ya mimi na mama yangu. Tulitumia Jumamosi iliyofuata tukifahamiana na sasa nahisi vizuri zaidi kuongea na mama yangu kuhusu jambo lolote.

Ninafuraha sana niliomba ushauri wa shangazi yangu siku hiyo kwa sababu mama yangu ndiye mtu nimpendaye sana duniani kote.