Je, huwa unahisi wivu?

Hizi hapa njia 4 za kukabiliana na hali hiyo!

Je, huwa unahisi wivu?

Springster inahusu wasichana kupiganiana haki zao. Hii inamaanisha kusaidiana, kutiana moyo na kushirikiana. Lakini natuseme ukweli, wakati wote hatuhisi kuwasaidia wasichana wengine. Wakati mwingine tunaingiwa na wivu na hiyo ni sawa. Kilicho muhimu ni jinsi unavyokabiliana na wivu na kuugeuza na kuwa na kujiamini na hisia chanya.

Wivu ni kule kuhisi kijicho juu ya mafanikio ya mtu mwingine, vitu alivyo navyo au nafasi aliyo nayo. Wivu hutufanya tuhisi hatuko salama na wakati mwingine hutufanya tumtendee mabaya yule mtu tunayemuonea kijicho. Aina hii ya hisia si nzuri kwetu na kwa hiyo tunahitaji kujifunza kuzidhibiti kwa njia ya ustadi.

Ukijiona unaingiwa na wivu kuhusu mtu mwingine, basi hii hapa njia ya kuugeuza na badala yake ujiamini.

1. Wewe ni wa kipekee.

Hakuna haja ya kuonea wivu mafanikio ya watu wengine, kwa sababu sisi sote tuna vipaji na talanta za kipekee. Ndani yetu sote mna mbegu za ukuu. Unahitaji tu kujifunza jinsi ya kuzifanyisha kazi.

2. Wewe hujashindwa

Ushindi wa mtu mwingine haumaanishi kwamba wewe umeshindwa. Sisi sote tuna uwezo wetu binafsi. Kwa kuwa tu msichana mmoja amefaulu shuleni kuliko wewe haimaanishi wewe ni wa chini kuliko yeye. Huenda huna uwezo wa kimasomo lakini unaweza kujishindia mambo mengine kama vile michezo, michezo ya kuigiza na kuwa na akili inayopenda biashara. Hebu chunguza uwezo ulio nao, ukijua uwezo wako utakuwa mtu anayejiamini zaidi.

3. Badili mtazamo wako.

Ukimwona mtu mwingine anafaulu katika kitu ambacho hata wewe ungependa kufaulu kwacho, basi wasiliana naye akuambie kile alichofanya hadi akafaulu. Badala ya kuona wivu, tumia mafanikio yao kama hamasa ya kukusaidia kufanya bidii zaidi. Watafute wakuhamasishe badala ya kujilinganisha nao kwa njia isiyokuwa nzuri.

4. Kuwa mwenyewe

Tumia muda ukiangazia maisha yako na uzidi kuwa mtu bora kuliko awali. Hakuna mtu aliyemkamilifu kwa hiyo kutumia muda wako kukua na kujiboresha ni bora zaidi kuliko kupoteza muda ukitamani laiti maisha yako yangefanana na ya mwingine. Kadri unavyojijua zaidi ndivyo zaidi utakavyohisi unajiamini zaidi.

Hatimaye kumbuka kuwa na subira maishani mwako. Maendeleo ya pole pole bado ni maendeleo na ushindi wa msichana mmoja haumaanishi wewe umepata hasara. Vivyo hivyo urembo wa msichana mmoja haumaanishi wewe una sura mbaya. Kuna fursa za kumtosha kila mtu!