Mambo yanapo onekana kuwa nje ya udhibiti wetu…

Usijilaumu. Fanya kwa kadri unavyoweza.

Mambo yanapo onekana kuwa nje ya udhibiti wetu…

Faiza, mwenye umri wa miaka 16 alivunjika moyo wakati duka la babake lilipofungwa na hakuwa na uwezo wa kulipa karo ya shule. Ingawa alikuwa na uwezo wa kujiandikisha kwa ajili ya mtihani wake wa mwisho, shule ilimwambia kuwa hangeweza kuendelea kuhudhuria na akajihisi mwenye kukata tamaa. Angewezaje kusomea mtihani ikiwa hangeweza kwenda shule? Faiza alihisi mfadhaiko na alikaribia kukata tamaa, wakati alipoona bango kwa jicho lake alipokuwa akipita pembezoni mwa maktaba yake ya mtaani. Bango hilo lilikuwa la msichana mdogo aitwaye Malala. Alikuwa ameshika kitabu, na maelezo hapo chini yalisema:

”Hebu tuchukue vitabu vyetu na kalamu zetu. Ni silaha zetu zenye nguvu zaidi. Mtoto mmoja, mwalimu mmoja, kitabu kimoja na kalamu moja inaweza badilisha ulimwengu.”

Msichana yule katika bango lile alionekana jasiri na mwenye bidii, na wakati huu Faiza alitambua kwamba anaweza kuwa kama msichana huyu pia. Faiza alipenda kusoma na haingembidi kukubali bahati mbaya ya babake kuharibu maisha yake ya usoni.

Mchana huo, Faiza alitembelea rafiki zake wawili wa karibu wa shuleni na kuwaambia wazo lake. Aliwauliza kama wangemfundisha walichojifunza shuleni kila alasiri. Kwa njia hiyo, marafiki zake wangeweza kupima hekima yao, na angeweza kujifunza mambo mapya.

Miezi michache iliyofuata ilikuwa migumu na kulikuwa na muda mwingi ambapo Faiza alijiuliza kama angeweza kuendelea. Hata hivyo, kila alasiri bila kukosa, Faiza alikutana na marafiki zake kwenye bustani na wasichana wale walijifunza. Watu walianza kuona jinsi wasichana wale walivyokuwa na bidii, na mwalimu wa mtaa huo aliyekuwa amestaafu alijitolea kumsaidia Faiza na maandalizi yake ya mtihani wa mwisho. Akivutiwa na kujitolea kwa Faiza na shauku yake ya elimu.

Mtihani ulipokaribia, Faiza alianza kuogopa, lakini kila wakati sauti hiyo hasi ilipomwambia kuwa hataweza, alikumbuka maneno ya msichana yule shujaa kwenye bango. Alipokumbuka maneno yale, aligundua kwamba alikuwa na uwezo wa kubadilisha ulimwengu wake.

Miezi michache baada ya mitihani yake, alipata barua aliyokuwa anaitumainia – aligundua kwamba alikuwa amefaulu mitihani yake. Faiza na familia yake walikuwa na furaha sana. Licha ya hali yake ngumu, Faiza alichagua kujiamini mwenyewe. Sasa ndoto yake ni kuwa mwalimu siku moja, na kuhimiza wasichana wengine wadogo kufuata ndoto zao.

Hadithi ya Faiza inatufunza sisi Springsters kwamba ingawa wakati mwingine mambo hayaendi kulingana na mipango, na vikwazo huonekana kutokea mahali popote, ni muhimu usijilaumu mwenyewe na ufanye kadiri uwezavyo.