Mbinu za kuweka akiba kwa ajili ya mustakabali wa thabiti

Mbinu za kuweka akiba kwa ajili ya mustakabali wa thabiti

Ninakaribia kumaliza masomo yangu na ninataka kujiunga na chuo cha biashara baada ya hapo ili kujifunza jinsi ya kuanzisha biashara yangu mwenyewe ya vipochi ninavyowatengenezea marafiki na wanafamilia wangu.

Wazazi wangu wanasema kuwa watanisaidia kujiunga katika chuo cha biashara, lakini kuwa nitapaswa kujilipia ili kupata masomo na pia kuanza kutoa msaada kidogo nyumbani katika kununua mboga na matunda.

Mimi hutumia pesa zangu visivyo, huwa sina akiba yoyote wakati ninapohitaji pesa - inaonekana ni kama kuna shimo katika mfuko wangu! Ninapenda pia kula vyakula vya mtaani pamoja na marafiki zangu panapowezekana - lakini ninajua kuwa jambo hili linanizuia kutoweka akiba yoyote.

Nilimwuliza mamangu kushiriki mbinu zake kuu za kuweka akiba zaidi na zilinisaidia kunitoa katika kiwango cha sufuri hadi kufikia lengo langu kwa wakati uliofaa;

Fahamu mapato na matumizi yako

Mamangu aliniambia kuwa ili kuanza na lengo la kuweka akiba, unahitaji kuangalia mapato na matumizi yako. Lengo la kuweka akiba ni kuwa na mapato zaidi yanayoingia kila mwezi kuliko matumizi. Iwapo mapato na matumizi yako yanalingana au hata matumizi yako ni ya juu kuliko mapato unayopata - hutafikia lengo lako.

Weka lebo kwenye anasa zako

Andika vitu ambavyo unatumia pesa zako kwavyo kwa mwezi mmoja kamili. Mwishoni mwa mwezi, chukua kalamu za rangi mbili na uangazie ‘mahitaji’ yako kwa rangi moja na ‘vitu vya ziada’ kwa rangi nyingine . Hitaji ni chakula cha msingi, afya au kusafiri kuelekea shuleni au kazini - kila kitu kingine ni ‘kitu cha ziada’. Kisha unaweza kuona ‘vitu vya ziada’ ambavyo unatumia pesa nyingi kwavyo na uweke malengo madogo ili utumie pesa kidogo. Lengo langu la kwanza lilikuwa ni kutonunua kinywaji baridi cha maziwa kwa mwezi wote mmoja.

Kuwa tayari kwa mapungufu

Maisha hutupa changamoto - na wakati mwingine changamoto hizi zina gharama zake. Kama miadi ya dharura ya daktari wa meno au kusafiri kwa ajili ya dharura ya familia. Jitayarishe kwa mapungufu kwa kuongeza 10% ya ziada kwenye lengo lako la kuweka akiba, kwa hiyo, iwapo kuna jambo litatokea, halitaathiri lengo lako kabisa.

Isitoshe, mamangu alinisaidia kununua kibubu ili kuweka akiba ya sarafu ndogo ndogo kila mwezi na kuifungua mwishoni mwa mwezi kama pesa zangu za ‘kujiburudisha’. Si pesa nyingi, lakini inaamisha kuwa ninaweza kupata chakula cha nje mara moja kwa mwezi pamoja na marafiki zangu - jambo linalonipa furaha!

Ninashukuru zaidi kwa ushauri wa mamangu kuhusu kuweka akiba! Kutokana na msaada wake niliweza kuweka akiba ya kutosha kila mwezi kwa ajili ya kozi na kwa sasa ninajiamini zaidi na pesa na kuwa nitaweza pia kuwa na pesa za kutosha ili kuchangia pia katika kulipa kodi nyumbani.