Hatari za kihisia za kufanya mapenzi mapema

Nina anaeleza hadithi yake

Hatari za kihisia za kufanya mapenzi mapema

Kuna hatari nyingi zilizopo ukiamua kufanya mapenzi katika umri mdogo. Nina alipoteza ubikira wake alipokuwa mchanga na ameeleza hadithi yake kwetu. Kama unafikiri uko tayari kufanya mapenzi na mpenzi wako, ni vyema kujua tajriba za wasichana wengine pia!

Mimi ni Nina na nilifanya mapenzi kwa mara ya kwanza nilipokuwa na miaka 16 pekee. Mpenzi wangu wa kwanza alikuwa kijana wa mtaa wetu. Baada ya miezi 3 ya kuwa pamoja alinihimiza tufanye mapenzi.

Kwa kweli nilifahamu kwamba sikuwa tayari kufanya mapenzi wakati ule, lakini kwa sababu nilitaka kujithibitisha kwake, nilikubali. Jambo la kusikitisha ni kwamba baada ya kilichotendeka kati yetu, alijitenga nami. Hakujibu jumbe zangu tena na ghalfa hakutaka kukutana nami tena. Nilihisi nimetumiwa sana.

Nilianza kufikiria sababu zilizonifanya kufanya mapenzi na nikafikiria jinsi ilivyonifanya nihisi. Baada ya kufanya mapenzi, nilihisi nimepoteza udhibiti wa mwili wangu mwenyewe. Nilianza kuhisi sina furaha, majuto yakanijia na nilijua nilihitaji kuzungumza na mtu kabla ya hisia hizi kuwa mbaya zaidi. Ushauri wangu ni daima hakikisha uko tayari na usifanye jambo ambalo haufurahii.

Niliogopa ningepoteza mwelekeo wa masomo yangu kabisa, kwa hivyo hatimaye nilizungumza na dadangu mkubwa kumjulisha kilichotendeka. Ni mtu ninayehisi ninaweza muamini kabisa na ninahisi vyema nikiwa naye. Aliniambia nisijichukie sana na akanisaidia kugundua kwamba kufanya mapenzi katika umri mdogo kuna hatari nyingi sana, kama kuwa na wasiwasi, majuto, hasira au kuhisi una hatia.

Kuna hisia nyingi sana zinazohusika unapofikiria kuhusu kufanya mapenzi kwa hivyo ni muhimu uzifahamu, sio hisia nzuri zote! Muhimu zaidi, fanya mapenzi wakati wewe na mpenzi wako mumezungumza na nyote mnahisi mko tayari kupiga hatua inayofuata.