Je, niko sawa?

Mbona kila mtu ananicheka?

Je, niko sawa?

Hivi majuzi nimekuwa na wakati mgumu shuleni. Wasichana wengine wameanza kuniambia mambo ya kikatili, kwa sababu nakaa tofauti nao. Nina takriban miaka 14 – lakini wamekuwa wakisema ninakaa kama nina miaka kumi!

Hili lilifanya nijiulize swali, je niko sawa? Mbona ni mimi tu niko tofauti? Kwa sababu tu sina matiti na chunusi, kila mtu ananicheka! Dhuluma ziliendelea kiasi kwamba sikutaka kwenda shule tena.

Siku moja nilijifanya ni mgonjwa. Nilikaa nyumbani siku nzima nikisoma hadithi za Springster mtandaoni. Nilisoma kwamba ubaleghe ni mchakato ambapo mwili mchanga unakuwa kiumbo na kuwa mwili wa mtu mzima wenye uwezo wa uzazi. Katika hatua hii miili huwa na umbo nzuri, mfupa wa kiuno hupanuka na huanza kupata hedhi zao. Watu tofauti hubaleghe katika umri tofauti. Kwa wastani wasichana hubaleghe kati ya umri wa miaka 10 – 14 lakini hii sio hali kila wakati, wasichana wengine hupitia mapema au kwa kuchelewa. Nilipata utulivu nilipogundua kwamba mimi ni binadamu timamu.

Kufahamu habari hii mpya kuhusu mwili wangu kulinifunza kutosheka na jinsi nilivyo na kuamini mchakato ule. Kukua ni safari na safari ya kila mtu ni tofauti. Kwa hivyo, badala ya kujilinganisha na watu wengine, shukuru kwa yale uliyonayo. Bila mwili wako hungekuwa na uwezo wa kupumua, kula au kutembea. Kwa hivyo ufurahie na uuthamini bila kujali unavyokaa. Kusoma kuhusu jinsi mwili wangu unavyobadilika kulinisaidia kujua ukweli na kukabadilisha mtazamo wangu.

Kwa hivyo, sasa ninapenda mwili wangu kama ulivyo na ninauzungumzia vyema. Hii ilinipaujasiri wa kwenda shule siku iliyofuata. Kama kawaida walianza kunikejeli, nilijitetea na nikawaambia kwa ujasiri, “Kwa sababu tu sijaanza hedhi zangu, sijamea matiti au kuongeza kilo au kimo haimanishi kwamba siko timamu. Ninapenda mwili wangu na ninafurahi kuuwacha ubadilike katika wakati wake wenyewe.”

Niligundua kwamba sikuhitajika kuyafikiria maneno yao mabaya – dhuluma zao sio shida kwangu, ni kwao. Baada ya kuzungumza nao hivi, waliwacha kunikejeli na wakajua kwamba nilifahamu mengi kuhusu ubaleghe. Walitaka kujua nilikotoa ufahamu huu wote na nikawaambia, “Kutoka Springsters!”