Rafiki yangu ni mwonevu

Hebu fikiria nilikabiliana vipi na hilo?

Rafiki yangu ni mwonevu

Rafiki yangu anayeitwa Shani ni mzuri sana, mwenye utani na anafurahisha. Tulikutana siku ya kwanza shuleni, na akajitolea kushiriki nami chakula chake cha mchana - tumekuwa marafiki wa karibu tangu siku hiyo!

Sasa katika mwaka wetu wa mwisho wa shule ya upili, Shani ameanza kuwaonea wasichana katika daraja lililo chini yetu. Anafanya vitu kama kuweka chakula kilichooza katika mifuko yao au kuficha vitabu vyao.

Kundi lote la marafiki zetu hawafurahii kuona hili likitendeka - lakini hakuna mtu anafanya chochote.

Siku moja nilishuhudia jinsi msichana mmoja aliyekuwa amemwonea alivyokuwa amekasirika na nikajua kwamba sitanyamaza tena.

Nilikuwa na wasiwasi kumwongelesha, lakini nilijua kama ningefanya hivyo kwa njia sahihi, angeweza kuniskiza.

Kwanza, nilihakikisha kuwa natafuta nafasi iliyo na faragha na ambayo Shani hangekuwa na wasiwasi. Sikumtaka adhani kwamba nilitaka kumpiga.

Kisha, nilitaka kumhakikishia kwamba nia ya kuzungumza naye ni kwa sababu ninamjali na pia najali urafiki wetu. Nilimkumbusha kuhusu jinsi tulivyofanya urafiki kwa sababu ya uzuri na usaidizi wake lakini sasa inanivunja moyo sana kutazama anavyowaonea watoto wengine shuleni. Kisha nikamwuliza kama ameona mabadiliko yoyote katika tabia zake na kama alikuwa akipitia shida yoyote.

Shani alionekana mwenye hasira kidogo kwanza, lakini nikampa nafasi ya kuelezea mtazamo wake kuhusiana na suala hilo. Nilihakikisha kuwa nimesikiliza bila kuingilia kati. Shani alikiri kwamba anadhani sababu ya kuwaonea wasichana katika daraja lililo chini yetu ni kutokana na hofu kwamba anaondoka shule mwaka ujao.

Hajui maisha yake yatakuwaje baada ya shule na anawaonea wivu kuwa wana muda zaidi wa kujitayarisha.

Baada ya kupiga gumzo, tulizungumzia kuhusu baadhi ya chaguo zinazopatika anapomaliza shule. Kwamba anaweza pia kupata masomo zaidi na kufanya kazi katika muda wa ziada hadi atakapopata jambo analopenda.

Kwa kuzungumza, unyanyasaji ulikoma na pia tulisulushisha sababu ya Shani kuwa na wasiwasi. Niliridhika sana kwamba niliongea - kwa kweli imetufanya kuwa marafiki wa karibu hata zaidi.

Natumai kwamba sasa unahisi kuwa unaweza pia kuwa na mazungumzo magumu pamoja na unaowapenda. Tafuta mahali patulivu, mkumbushe mtu huyo kwamba nia ya kufanya hivyo ni kwa sababu unajali uhusiano wenu na kisha uhakikishe umesikiliza anayokwambia.