Nilishiwa na Visodo…

Na sikuwa na pesa za kununua vingine

Nilishiwa na Visodo…

Vipi dada!

Jina langu ni Naobi, wiki iliyopita ilikuwa na shughuli nyingi! Nimekuwa nikisoma kwa bidii kwa ajili ya mitihani yangu ya mwisho. Nilikuwa na hofu sana sikutaka kufeli ili niweze kuenda darasa lililofuata.

Ijumaa asubuhi, niliamka kwa furaha, tayari kwa mitihani miwili ya mwisho. Nilipiga meno mswaki, nikaosha uso na nikaoga. Nilipokuwa nikioga niligundua nilikuwa nimeanza hedhi zangu!

Nilitazama mfuko wangu na nikagundua nilikuwa nimemaliza visodo. Niliangalia sanduku langu ambapo mimi huweka pesa nilizoweka akiba lakini sikuwa na pesa za kutosha kununua visodo vipya. Kwa hivyo, badala yake nilivaa nguo safi na suruali mbili na nikaenda shule.

Nilimaliza mtihani wangu wa kwanza kwa mafanikio. Lakini mchana nilipata mtiririko mzito na nguo ile haingeshikilia damu tena. Nilihitaji kubadilisha haraka iwezekanavyo!

Niliogopa sana kuomba rafiki msaada kwa sababu niliambiwa kuweka hedhi siri. Nilidhani watu wangenihukumu kwa kuwa na hedhi. Lakini wajua vipi wasichana? Mama yangu daima aliniambia “woga ni wazo mbaya la kitu kinachokuja ambacho bado hakijatendeka.” Kwa hivyo kama ninaweza kuwa na mawazo ya matokeo mabaya, ninaweza kuwa na ya matokeo mazuri.

Badala ya kufikiria watu watanihukumu kwa kuwa na hedhi, nilianza kujiambia kwamba hedhi ni kawaida na rafiki wa kweli angekuwa radhi kunisaidia. Jambo mbaya zaidi wangefanya ni kukataa, lakini tena ningemuuliza mtu mwingine. Hakuna ubaya wowote! Nilijiambia kimoyomoyo mara 5 tena nikahesabu 5,4,3,2,1 na nilipofika 0 nikaamua. Nilimuendea rafiki yangu Asia na nikamuomba kisodo.

Kwa sababu sikuruhusu woga unishike niliweza kuzungumza na Asia na akanipea visodo 3 vya kunisaidia kwa siku kadhaa zaidi na akaniambia kwamba kuomba kisodo sio jambo la kuonea aibu. Hakuna haja ya kujificha wakati uko na hedhi. Hedhi ni sehemu ya kawaida ya kukua. Kawaida kama kuwa mrefu au kumea nywele.

Asia pia alinishauri niweke pesa kando kuhakikisha nina pesa za kutosha za kununua visodo na kuwa na vya ziada kwa rafiki atakayehitaji.

Baada ya kubadilisha, nilifanya mtihani wangu wa mwisho nikiwa na furaha. Ninafurahi sikuruhusu woga unizuie. Wakati mwingine nikiwa na haja sitajali sana kuhusu fikra za watu wengine. Nitakuwa jasiri na niombe msaada mara moja.