Niliona aibu shuleni

Sikuwa tayari kwa yaliyotokea

Niliona aibu shuleni

Nilikuwa nimefikisha miaka 13 na nikapata hedhi yangu kwa mara ya kwanza mwezi uliopita. Nilipoona damu kwenye chupi yangu kwa mara ya kwanza nilishangaa, lakini sikuogopa kwa kuwa mamangu alikuwa ameniambia hapo awali kwamba hedhi yangu itaanza baada ya mimi kuvunja ungo. Nilimwambia yaliyotendeka na akanipa pakiti ya visodo na akanionyesha namna ya kuviweka kwenye chupi yangu. Ilikuwa hali geni kwangu na ilinichukua muda kuzoea, lakini mwishowe nilizoea.

Mgeni asiyetarajiwa

Mwezi mmoja baadaye, nilikuwa kwenye chumba cha maankuli na marafiki zangu nilipoanza kuhisii maumivu kwenye sehemu ya chini tumboni. Nilidhani nimekula kitu kibaya lakini iliishia kuwa zilikuwa dalili kwamba ningepata hedhi yangu na sikuwa tayari.

Niliihisi damu ikitiririka kwenye miguu yangu, na nikajua ilimaanisha sketi yangu huenda ilikuwa na madoa ya damu. Singeinuka. Nilifedheheka. Kwa nini hili likatendeka kwangu katika chumba cha maankuli kukiwa na watu wengi hivi kando yangu?

Fedheha? Aibu? La. Sio moja kati ya haya!

Nililazimika kwenda nyumbani mapema kuoga na kubadilisha chupi yangu. Nilimwambia mamangu kilichotendeka na nilihisi kulia kwa kuwa nina uhakika watu waliniona. Lakini mamangu alinihimiza kuwa hakuna chochote cha kunipa fedheha.

Aliniambia ”mambo yanafedhehesha kwa sababu ya hadithi tunazojiambia akilini mwetu kuhusu hali hii” Aliniambia nisiwaze vibaya kuhusua hali yangu. Badala yake napaswa kujipa changamoto ya kuwaza mazuri kuhusu kilichotendeka. Mawazo kama “Hedhi ni jambo la kawaida” na “ hali ngumu hutokea lakini jinsi unavyokabiliana nazo ndio muhimu".

Kuwa mjanja kuhusu hedhi

Mamangu aliniambia kuwa kupata hedhi bila kutarajia hutokea kwa wasichana wengi wanapoanza. Unahitajika tu kuwa mjanja kuhusu kuweka rekodi ili kuhakikisha uko tayari kila mara.

Hmm, kuweka rekodi ya hedhi yangu? Sikuwahi liwazia hilo. Kwa hivyo nilitafuta kalenda maalum ya hedhi yangu na sasa kila mwezi mimi huhesabu siku ya kwanza ya kutoa damu kama siku 1 kisha nahesabu siku 28 baadaye ili kuona hedhi ifuatayo itakuwa lini. Kwa wasichana wengi, kipindi kabla ya hedhi ni siku 21 hadi 35, kwa hivyo ninahakikisha nina visodo kuanzia siku ya 21.

Kwa hivyo wasichana, kumbukeni, hedhi sio kitu cha kukutia fedheha. Kila mara kuwa na kisodo na uweke rekodi ya hedhi yako ili ujipange. Na iwapo bado jambo litaenda mrama, usijali! Fikiri haraka na uchukue hatua.