Mama katika umri wa miaka 16

Hadithi yangu haijaisha bado

Mama katika umri wa miaka 16

Hamjambo wasichana,

Naitwa Khadija na mimi ni mmoja kati ya watoto wanane waliozaliwa na baba na mama wanaotupenda. Babangu alikuwa na kazi na alihakikisha sote tuna maisha mazuri. Lakini alipoaga dunia, maisha niliyoyazoea yalifika kikomo.

Katika nchi yetu, mjane hana haki ya kuishi katika nyumba ya bwanake. Kwa hivyo wajomba wangu walitulazimisha kuondoka kwetu na ikatubidi kuhamia shamba ndogo katika kijiji alikotoka mamangu. Nilikaa nyumbani bila ya kwenda shuleni ili kuisaidia familia yangu kutengeneza matofali ili kujengea nyumba mpya. Maisha yetu yalikuwa juhudi za kutimiza mahitaji yetu ya kila siku.

Lakini licha ya uchovu au njaa niliyokuwa nayo, nilijikaza shuleni. Nilijiambia nitulie na nizingatie malengo yangu. Kila muda wa ziada niliokuwa nao baina ya shughuli za kulima na kuosha nyumba, nilisomea mitihani yangu ili nifuzu kuingia sekondari. Juhudi zangu zilizaa matunda nilipopita mtihani wangu wa mwisho vyema kwa kupata alama nzuri kabisa. Lakini hatungemudu karo ya sekondari. Nilingoja mwaka mzima ili nirudie mtihani kwa matumaini kwamba ningepata ufadhili ili kujiunga na shule ya mabweni ya wasichana - na nikafanikiwa kuupata!

Siku moja, wanafunzi wenzangu walinishawishi kwenda ufuoni. Huko ndiko nilikutana na mvulana mzuri sana. Baada ya siku hiyo tulianza kuwasiliana na hatimaye akaniomba niwe mchumba wake Nikakubali na tukawa wachumba! Alinishawishi kufanya mapenzi naye na miezi michache baadaye nikawa mja mzito.

Hakuna mtu aliyewahi kuniongelesha kuhusu ngono hapo mbeleni. Nilichanganyikiwa sana. Sikujua hata mipira ya kondomu ni nini au namna ya kuitumia, nilimwamini kunikinga. Ilikuwa vigumu kukubali kwamba nilikuwa mja mzito. Mamangu alikasirika sana. Nami pia nilikasirika. Nilikuwa na mpango wa kukamilisha masomo yangu lakini mimba ilimaanisha nilipoteza ufadhili wangu.

Nilipojifungua mtoto wa kiume, nilijawa na upendo na furaha kwamba nilileta kiumbe kipya duniani. Maisha yalikuwa magumu bado lakini tuling’ang’ana. Baada ya takriban mwaka mmoja, mwanaume mmoja alikuja nyumbani kwetu – aliniarifu kwamba alifanya kazi na Shirika la AIDS Support ambalo huwasaida akina mama wachanga ambao hawajaolewa kurejea shuleni na kupata elimu.

Aliniarifu kwamba ili nifuzu ningehitajika kufanya kazi kama mshauri na kuwaambia wasichana wengine kuhusu maisha yangu ili wajifunze kutokana na tajriba zangu na wasiogope kujieleza wasipotaka kushiriki jambo lolote. Nikaitikia! Nilishukuru kwa nafasi ya kuendelea na masomo yangu na kuwasaidia wasichana wengine kama mimi.

Mwanangu sasa ana miaka 3. Imesalia miaka miwili tu kabla nifuzu sekondari. Nimepitia mengi lakini hadithi yangu haijaisha bado. Kutoka shuleni na kupata mtoto ilikuwa ni sura mojawapo tu katika maisha yangu. Najua nikiendelea kufanya bidii na nisipokata tamaa nitashinda vizuizi vyovyote.

Ijapokuwa watu huenda wakafikiri mambo mabaya kunihusu kwa kujifungua mapema, ninajivunia kwamba mimi ni kielelezo kwa wasichana wengine. Nafikiri ni muhimu niwahimize wale ambao pia wana watoto warejee shuleni, na wawasaidie wasichana kuepuka mimba za mapema.