Nywele mwilini, haziijalishi!

Je, hadithi za wasichana hawa zinafanana na yako?

Nywele mwilini, haziijalishi!

Nywele zinaweza kuchangia pakubwa katika maisha yetu. Kuanzia nywele zilizo vichwani mwetu hadi nywele hizo chache kwenye vidole vyetu vya miguu. Siku nyingi zinaweza kupita bila kuziwazia - lakini nywele zinapoanza kukua katika sehemu mpya inaweza kuwa vigumu kuziondoa kwenye fikra zetu.

Leo tunashiriki hadithi za wasichana ambao walikubali jinsi nywele zilivyojitokeza kwenye miili yao.

Ode aliporudi shuleni, aligundua kwamba wasichana wengi walikuwa wamenyoa nywele kwenye miguu yao kwa mara ya kwanza. Ode alianza kuhisi wasiwasi na kuwauliza wazazi wake kama angeanza kunyoa nywele zake pia. Lakini wazazi wa Ode walidhani kuwa bado angali mdogo sana, lakini walimwambia Ode kwamba ikiwa hatua hiyo ni ya kujitakia na ikiwa ingemfanya ahisi sawa basi angeweza kunyoa.

Kadiri Ode alivyowaza jambo hilo, alijua kuwa anataka kufanya hivyo mradi tu afanane na marafiki zake. Kwa hivyo, badala yake aliendelea kusalia na nywele miguuni mwake hadi atakapofanya chaguo bila shinikizo. Hadi sasa, yeye hukata nywele tu wakati unaofaa na kamwe hahisi shinikizo la kutaka kufanana na wengine.

Aminata amekuwa akinyoosha nywele zake kabla ya kwenda shule kwa miaka mingi, ingawa kitendo hiki huwa kinaharibu nywele zake. Alidhani kufanya hivyo kutamfanya afanane na wasichana wengine shuleni ambao walikuwa na nywele ndefu, zilizonyooka. Siku moja alikuwa amechelewa sana na akashindwa kunyoosha nywele zake. Alidhani kila mtu shuleni angetambua tofauti kubwa na atoe maoni.

Hakuna hata mtu aliyegundua na isitoshe watu walikuwa wanasema kwamba ana kitu fulani siku hiyo kilichokuwa kinamfanya apendeze lakini hawakuwa wanatambua ni nini. Kuanzia siku hiyo Aminata aliacha kunyoosha nywele zake na kuziachilia ziwe na mwonekano wa asili.

Katika shule ya upili, Gemma alianza kupata nywele nyeusi kwenye mdomo wake wa juu na akaanza kuwaonea wivu wasichana ambao hawakuwa na nywele kama hizo. Alipozinyoa au kuzipaka nta, nywele ziliendelea kukua hata zaidi, lakini aliendelea kufanya hivyo.

Siku moja alipokuwa na mpenziwe, akakumbuka kwamba alisahau kunyoa nywele zile. Gemma akaingiwa na hofu kwamba mpenzi wake angeweza kugundua na kumuaibisha. Lakini hakugundua. Aliacha kukata nywele zake na hatimaye alizungumza na mpenziwe kuhusu nywele hizo, naye mpenziwe akasema - hizo nywele fupi sana ambazo hazina madhara yoyote mabaya. Hiyo ni sehemu nyingine tu ya mwili wake - na yeye ni mrembo. Gemma hakuwahi kumdharau mpenziwe kwa sababu alikuwa na nywele usoni, hivyo akagundua kuwa haingekuwa haki kwa mpenziwe kumdharau pia.

Kila msichana anayo hadithi tofauti, hivyo usiwahi kulinganisha mwili wako na wa mtu mwingine. Cha muhimu zaidi ni sifa tulizonazo ndani mwetu na sio mwonekano wetu.

Kwa hivyo ikiwa unamwona rafiki akiwa na wasiwasi kuhusu nywele katika mwili wake mwambie kuwa ni jambo la kawaida na umtie moyo.